Abstract
Ikisiri Utafiti huu unalenga kuchunguza athari za mbinu ya Jigsaw katika kuboresha ufahamu wa kusoma miongoni mwa wanafunzi wa Libya wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni katika Chuo Kikuu cha Tripoli. Ufahamu wa kusoma ni stadi muhimu katika ujifunzaji wa lugha, lakini changamoto za motisha na ushiriki mdogo mara nyingi huathiri wanafunzi. Mbinu ya Jigsaw ya ujifunzaji shirikishi iliyoanzishwa na Elliot Aronson, huwapa wanafunzi majukumu ya kusoma sehemu tofauti za matini na kisha kushirikishana maarifa yao ndani ya vikundi ili kujenga uelewa wa pamoja wa maandishi. Utafiti huu ulitumia mbinu mseto ya ukusanyaji data ili kupata picha kamili ya athari za mbinu ya Jigsaw. Vipimo vya kabla na baada ya somo vilitumika kupima maendeleo ya wanafunzi, uchunguzi wa darasani uliangazia ushiriki na ushirikiano, huku hojaji fupi zikikusanya mitazamo ya wanafunzi kuhusu mchakato wa kujifunza. Matokeo yalionyesha kuwa wanafunzi waliotumia mbinu ya Jigsaw waliboresha ufahamu wao wa msamiati na maana ya matini, huku pia wakiongeza kiwango cha ushiriki na kujiamini katika mijadala. Ushirikiano wa kikundi ulionekana kuongeza motisha na kupunguza hofu ya kushiriki kwa wanafunzi wengi, jambo muhimu katika ujifunzaji wa lugha za kigeni. Utafiti huu unatoa mchango muhimu katika mjadala wa kimataifa kuhusu mbinu bora za kufundisha Kiswahili katika mazingira yasiyo ya lugha asilia. Aidha, unathibitisha kuwa mbinu shirikishi kama Jigsaw zinaweza kukuza stadi za usomaji na kuongeza ushiriki wa wanafunzi wanaojifunza lugha za Kiafrika.
